Kiungo N’golo Kante ameripotiwa kwamba muda wowote atakamilisha dili lake la pesa nyingi la kujiunga na klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia akitokea Chelsea.
Dili hilo lilitarajiwa kukamilika jana Jumatano (Juni 14), huku akitimkia zake huko Saudi Arabia bure kabisa baada ya mkataba wake wenye thamani ya Pauni 290,000 kwa wiki kufika tamati huko Stamford Bridge mwishoni mwa mwezi huu.
Lakini, sasa ataachana na The Blues baada ya miaka saba ili kwenda kupiga mshahara mrefu, Pauni 1.7 Milioni kwa wiki, ikiwa ni mara sita ya kiwango ambacho amekuwa akilipwa huko Stamford Bridge.
Mwandishi Fabrizio Romano alituma ujumbe kwenye Twitter: “Nakala zote zimeshasainiwa kati ya N’Golo Kante na Al Ittihadhivyo dili lake litatangazwa muda wowote. Mshahara wa Kante utakuwa kati ya Pauni 86 milioni na ameshafanyiwa vipimo vya afya. Inathibitishwa, huu ni mwisho wa zama zake Chelsea.”
Mkwanja wa Kante unaripotiwa kwamba utahusisha mshahara, haki ya taswira zake na dili za matangazo.
Kiungo huyo Mfaransa alijiunga na Chelsea kwa ada ya Pauni 30 milioni akitokea Leicester City mwaka 2016 na tangu wakati huo alicheza mechi 269 katika kikosi hicho cha Stamford Bridge.
Hata hivyo, kwa msimu uliopita, alicheza mechi tisa tu kutokana na kuwa na majeruhi ya misuli ya mara kwa mara.