Rapa Kanye West ni kama kwasasa focus yake kubwa imehamia kwenye namna ya kugeuza malumbano (bifu) baina yake na msanii Drake kuwa sehemu ya kurejesha kwa jamii kwa kuanza na kumsaidia Larry Hoover kutoka Gerezani .

Mapema usiku wa kuamkia leo Nov 9, 2021. Kanye ameweka kipande cha video chenye kumuonyesha akizungumza kuhusu kutaka suluhu kati yake na rapa Drake na ikiwezekana washiriki pamoja kwenye tamasha maalum litakalofanyika Disemba 7, 2021.

Katika video hiyo, Kanye anaonekana akisoma maelezo aliyokuwa akiyazungumza kutoka kwenye simu yake mkononi  akitaka amani na Drake na kuelezea hisia zake ili kukomesha ugomvi wao.

“Ninatengeneza video hii ili kushughulikia mambo yanayoendelea kati yangu na Drake. Wote mimi na Drake tumerushiana maneno kwa pamoja lakini nadhani ni wakati wa kupumzika. Ninamwomba Drake mnamo Desemba 7 ajiunge nami kwenye jukwaa kama mgeni maalum ili kuzishirkisha albamu mbili kubwa za mwaka, moja kwa moja huko Los Angeles lengo kuu likiwa ni kupambania Larry Hoover aachiliwe kutoka jela,” Ye alisema.

“Ninaamini tukio hili halitaleta ufahamu kwa sababu yetu, lakini litathibitisha kwa watu kila mahali ni kiasi gani tunaweza kutimiza tulitakalo, tunapoweka kiburi chetu kando na kukusanyika pamoja.” Aliongeza Kanye.

Katika Video hiyo Kanye anaonekana akiwa amesimama na mmoja wa promota maarufu wa wasanii nchini Marekani J,Prince ambaye naye kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram ameweka bayana kiwango cha busara na uelewa mkubwa alio nao Kanye west kwenye jambo hilo hasa baada ya mapokezi ya salamu na ujumbe wa Larry Hoover ambao J, Prince alimfikishia Kanye.

“Nilikutana na @kanyewest jana usiku huko Htown kwenye kanisa la Rothko Chapel. Haikuwa katika mipango yangu kukutana naye huko lakini lazima niseme ninafurahi kwamba sikuruhusu mahali pa ibada kwa Mungu kupotosha mkutano wetu. Itakuja wakati maishani ambapo sote tunapaswa kukumbatia fikra chanya, Kufikiri kwa muda kunatuweka kwenye mzunguko wa wakati mwingine kuchanganyikiwa, kulipiza kisasi, mauaji na mambo ya giza ambayo yanakupeleka mahali pabaya kuliko utumwa. Wanaofikiria harakati huota kesho bora, picha kubwa zaidi, chaguzi za maisha marefu na kujinyenyekeza ili kusamehe. Hawaruhusu woga na kiburi kudumaza ukuaji wao, na daima wanatafuta mema katika kila hali na hapo ndipo viongozi hutenganishwa na wafuasi. Kwa hiyo nilikutana na Ye ili kuwasilisha ujumbe kutoka kwa kaka yangu Larry Hoover ambaye alisema angependa kuona amani kati yao wawili Kanye na Drake, alipokea hili vizuri na akasema asante kwa sababu hakuwahi kuwa na mtu yeyote ambaye alimketisha na kumweleza mambo jinsi nilivyofanya. Natarajia sote tufanye kazi pamoja kwa umoja ili kuinua jamii zetu kote ulimwenguni”. Aliandika J, Prince kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Larry Hoover aliyemtuma J, prince kufikisha ujumbe wa amani kati ya Drake na Kanye ni mmoja wa waanzilishi makundi ya kihalifu maarufu (Gangster Disciples) huko nchini Marekani, anayetumikia kifungo cha maisha Gerezani tangu mnamo mwaka 1973, kwa makosa kadhaa yakiwamo ya Mauaji, uvamizi, Biashara ya dawa ya kulevya nk.

Ayoub Lyanga kutibiwa Afrika Kusini
Bilioni 18 kuanza ujenzi wa Barabara 3 Geita