Mazoezi ya mara kwa mara ya kupiga Penati ndio sababu iliyomsukuma Beki wa Kulia wa Simba SC Shomari Salum Kapombe kuchukua jukumu la kupiga Mkwaju wa Penati, wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Simba SC ilikua mwenyeji wa mchezo huo wa ‘Kundi D’ Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam na kuibuka mbabe kwa mabao 3-1.
Kapombe aliamua kuchukua maamuzi ya kupiga Mkwaju huo wa Penati, baada ya Yusuf Muhilu kuchezewa Faulo katika eneo la hatari na Mlinda Lango wa ASEC Mimosas.
Beki huyo ambaye aliwahi kucheza soka nchini Ufaransa amesema, aliamua kwenda kupiga Penati hiyo, kutokana na kufanyia mazoezi mara kwa mara, bila kuhofia jukumu hilo.
Amesema kila siku baada ya mazoezi ya kawaida kumekuwa na muda wa kupiga Penati na hilo ndilo lilimpa ujasiri wa kwenda kubeba jukumu hilo.
“Tunafanya mazoezi ya kupiga Penati kila siku, lakini katika mchezo ule tulihitaji kushinda ile Penati kwa sababu dakika zilikuwa zimekwenda sana na tulihitaji ushindi nyumbani.”
“Wakati nakwenda kupiga nilikuwa namuomba Mungu anisaidie nipate, pili nilikuwa naifikiria timu, familia yangu pamoja na mashabiki ambao walikuwa wanahitaji furaha kwa wakati ule, namshukuru Mungu nilifanikiwa,” amesema Kapombe.
Tangu kuanza kwa msimu huu, wachezaji wengi wa Simba wamekosa Penati, akiwamo John Bocco, Erasto Nyoni, Meddie Kagere na Chris Mugalu.