Beki wa upande wa Kulia wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Shomari Salum Kapombe amesema kikosi chao kimejiandaa vizuri kuelekea mchezo wa Kesho Jumapili (April 17), dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Simba SC itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikihitaji ushindi ambao utaiweka katika mazinguira mazuri kabla ya kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili mwishoni mwa juma lijalo Afrika Kusini.
Kapombe amesema wachezaji wamejiandaa vizuri na wapo tayari katika kupata ushindi kwa mchezo wa kesho Jumapili (April 17), japo amekiri mchezo utakuwa mzuri na mgumu kwa timu zote mbili.
“Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya kuikabili Orlando Pirates, tunajua mchezo utakua mgumu kwa muda wote, lakini kwa maandalizi tuliopewa na Kocha wetu ninaamini tutapambana ili kuhakikisha tunapata ushindi mzuri kabla ya kwenda Afrika Kusini kwa mchezo wa Pili.” Amesema Kapombe
Wakati huo huo Kocha Mkuu wa Simba SC Franco Pablo Martin amesema kama timu wapo vizuri kuanzia Benchi la Ufundi na wachezaji kwa ujumla, kufuatia maandalizi mazuri walioyafanya kwa muda wa juma moja.
Pablo amesisitiza kuwa: “Ni wazi klabu ya Simba imekuwa na rekodi nzuri inapocheza nyumbani kwa hiyo wachezaji na timu kwa ujumla wanakila sababu ya kutumia faida ya uwanja wa nyumbani na kuhakikisha wanashinda pambano hilo.”
Katika hatau nyingine Kocha Pablo ametoa rai kwa mashabiki wa Simba SC kujitokeza kwa wingi waujaze uwanja wa Benjamin Mkapa siki ya kesho ili kuwasapoti wachezaji katika mchezo huo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.