Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. George Mkuchika anatarajia kuhudhuria sherehe za kuapishwa na kutambulishwa kwenye jumuiya za Kimataifa kwa Mfalme Nahurito wa Japan Oktoba 22, 2019.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jijini Dodoma kwa vyombo vya Habari na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Kapt. Mkuchika atahudhuria sherehe hiyo kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli.
“Mheshimiwa Mkuchika anamwakilisha Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye alialikwa katika sherehe hizo na Waziri Mkuu wa Japan Mheshimiwa Shinzo Abe,” imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa katiba na sheria za kifalme za Japan Mfalme Nahurito amerithi kiti cha Baba yake Mfalme Akihito ambaye alitangaza kujiuzuru rasmi nafasi yake April 30, 2019 kutokana na umri wake kuwa mkubwa sanjari na kusumbuliwa na matatizo ya kiafya.
Mfalme Nahurito rasmi alichukua madaraka hayo Mei mosi 2019 ambapo Waziri Mkuchika na ujumbe wake wanatarajia kuondoka nchini Oktoba 19, 2019 na kutazamiwa kurejea nchini Oktoba 24, 2019.