Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amemkabidhi cheti cha heshima Kardinali Pengo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake ndani ya kanisa na katika shughuli zingine za kijamii ambapo amesema Kardinali Pengo ni kiongozi wa mfano.

Dkt. Mpango amesema hayo wakati wa sherehe ya kuadhimisha miaka 50 ya Upadre wa Kardinali Pengo ambapo ameeleza kuwa katika kutambua mchango wa kiongozi huyo wa kidini, serikali itaendelea kushirikiana bega kwa bega na viongozi wa dini katika kuijenga nchi yenye amani na mshikamano.

“Kardinali Pengo amewahudumia wananchi bila ubaguzi, anapoazimisha Miaka 50 ya utumishi wake Viongozi wa Serikali Wana mengi ya kujifunza kutoka kwake ikiwa ni pamoja na uvumilivu na hekima katika kuwaongoza watu,” amesema Dkt. Mpango.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Thadaeus Ruwa’ichi amebainisha kuwa kanisa linajivunia kumpata kiongozi huyo na kwamba kazi zake zitabaki kuwa alama isiyofutika ndani ya jimbo hilo.

Akiwashukuru viongozi mbalimbali wa kiserikali na waamini walioungana naye katikasherehe hiyo Kardinali Pengo, amesema anaamini ushirikiano alioupata kwa waamini na viongozi wa Serikali katika awamu zote za uongozi uliopita zimekuwa chachu ya maendeleo katika kanisa na jamii kwa ujumla.

Kardinali Pengo alikabidhiwa Jimbo Kuu la Dar es Salama mwaka 1992 likiwa na Parokia 20 na mpaka anastaafu kama Askofu Mkuu ameacha Jimbo hilo likiwa na Parokia 118.

Waziri amsimamisha kazi mhandisi stendi ya Mwenge
Kardinali Pengo umelifanya Jimbo la Mpanda kujitegemea -Askofu Nzigirwa