Kuendelea kwa Ligi Kuu na Ligi za madaraja ya chini msimu wa 2019/20 kutategemea maelekezo ya Serikali kuhusu usalama na tahadhari ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Serikali ilizuia shughuli zote za mikusanyiko ikiwamo za kimichezo kwa siku 30 kuanzia Machi 17 ikiwa ni kuchukua tahadhari ya mlipuko wa ugonjwa wa corona unaotikisa dunia.

Zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kukamilika kwa tarehe hiyo iliyotangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Karia alisema michezo ya ligi haitaendelea baada ya kipindi hicho hadi watakapopewa maelekezo ya kufanya hivyo kutoka serikalini.

Hivi karibuni Shirikisho la Soka la duniani FIFA, lilitaka wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukingoni kutoondoka kwenye timu zao hadi pale ligi ya nchi husika itakapomalizika, waraka ambao Karia amesema unaeleweka.

Hali halisi inaonekana, kwenye Ligi yetu hakuna mchakato wowote unaoendelea hadi pale Serikali itakapotoa maelekezo.

Licha ya hivi karibuni baadhi ya wadau kushauri Ligi Kuu ifutwe na wengine kutaka ichezwe bila mashabiki kipindi hiki cha tahadhari ya corona, Karia alisema hayo ni mawazo yao na si msimamo wa TFF.

Katika kuhakikisha kwamba hakutokei mkanganyiko wa taarifa alitoa maelekezo kwa viongozi wa TFF akiwataka wasizungumze chochote kuhusiana na ligi hadi pale Serikali itakapotoa msimamo juu ya janga la Corona.

TFF itatoa msimamo baada ya kupata maelekezo kutoka serikalini na si vinginevyo.

Kabla ya kauli ya Karia, baadhi ya wadau walitoa maoni yao wengine wakishauri ligi ya msimu huu ifutwe na kusiwe na timu za kushushwa daraja na kwamba bingwa wa msimu uliopita aendelee kuwa bingwa.

Wadau wengine walipingana wazo hilo na kushauri ligi isimame kwa muda usiojulikana hadi pale upepo wa corona utakapopita iendelee ilipoishia.

Ligi Kuu iliposimashwa kati kati ya mwezi uliopita, Simba ilikuwa inaongoza kwenye msimamo na ilikuwa inahitaji kushinda mechi tano kati ya 10 ilizobaki ili kutangazwa bingwa kwa mara ya tatu mfululizo.

Timu za Singida United, Mbeya City, Mbao na Alliance zilikuwa zinachuana mkiani wakati Gwambina ilikuwa inahitaji kushinda mechi moja kupanda kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Julio apongeza hisani ya GSM
Simba SC kuishtaki Young Africans TFF, FIFA