Serikali Nchini, imetoa wito kwa washiriki wa Kongamano la Nishati wakiwemo Mawaziri, Watunga Sera, Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi, Wafanyabiashara na Viongozi mbalimbali wa Makampuni kutoka ndani na Nje ya Tanzania wa mwaka 2023, kutumia mazingira rafiki yaliyopo Tanzania ili kuwekeza katika Sekta hiyo ya Nishati.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman wakati wa hafla ya kufunga Kongamano hilo la siku mbili lililofanyika Septemba 20–21, 2023 jijini Dar es Salaam, na kuongeza kuwa Tanzania ni nchi yenye kila sifa ikiwepo Amani na Utulivu.
Amesema, “kwa wale wageni ninawaalika kuja kuwekeza Tanzania kama mnavyojua kwa miongo kadhaa sasa Tanzania tumekuwa kinara wa Amani, Tanzania ni moja kati ya nchi zenye utulivu wa kisiasa Duniani, mliopo hapa mmepata nafasi ya kujadili na kutafuta ufumbuzi na ubunifu wa nishati katika kuiendeleza Sekta hii maarufu.”
Akiongelea upande wa Zanzibar, Othman amesema pia imejiwekea Mikakati Maalum ya Uwekezaji, hususan Sera za Uchumi wa Buluu, ambao aliutaja kuwa ni tegemeo visiwani humo na kwamba inahitaji Wawekezaji na Washirika wa Kimataifa watakaowezesha Mabadiliko ya Kweli katika Sekta za Nishati, Gesi Asilia na Mafuta kupitia Mapinduzi muhimu ya Teknolojia.
Kongamano la Nishati Tanzania kwa mwaka 2023, limejumuisha Wajumbe kutoka takriban Nchi 93 Duniani ambao pamoja na mambo mengine wamejadili na kuweka mapendekezo, juu ya Usambazaji wa Gesi Asilia (LNG).
Mengine ni Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP), Ubunifu wa Nishati Endelevu, Mbinu Mbadala katika Uzalishaji wa Nishati, na Namna bora ya Ufadhili wa Miradi Mikubwa ikiwemo ya Nishati, ndani na nje ya Bara la Afrika.