Mshambuliaji wa Ufaransa Karim Benzema Rasmi ametangaza kustaafu kuitumikia Timu ya Taifa ya nchi hiyo, baada ya Fainali za Kombe la Dunia 2022, zilizofikia tamati juzi Jumapili (Desemba 18) nchini Qatar.
Benzma ambaye alishiriki kwenye vita ya kuivusha Ufaransa wakati ikiwania kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2022 ikitokea Barani Ulaya, hakufanikiwa kuwa sehemu ya kikosi cha mwisho kilichopambana nchini Qatar, kufuatia majeraha yaliyomuadama siku moja kabla ya kuanza kwa Fainali hizo.
Mshambuliaji huyo ambaye atafikisha umri wa miaka 35 Jumatatu ya Juma lijalo, ametangaza kuastaafu kuitumikia Les Bleus, akiacha kumbukumbu ya kucheza michezo 97 na kufunga mabao 37.
“Nimeandika Historia yangu na ninajua kuna makosa niliwahi kuyafanya nikiwa na Timu hii, lakini sijali kwa sababu lipo la kujivunia wakati wote nilipokuwa na Timu hii, leo ninatangaza rasmi kustaafu kuitumikia Timu hii.”
Ujumbe huo wa Benzema ulijibiwa katika kurasa za Mitandao za Shirikisho la Soka la Ufaransa ‘FFF’: “Ahsante Benzema”.
Benzema ambaye ni Mshambuliaji Tegemeo katika kikois cha Mabingwa wa Soka nchini Hispania na Barani Ulaya Real Madrid, aliwahi kuachwa katika kikosi cha Ufaransa kwa miaka sita, kufuatia sakata la kuhusiska na Skendo za kusambaza Picha Chafu mitandao za mchezaji mwenzake Mathieu Valbuena.
Alianza kuonekana tena kwenye kikosi cha Timu hiyo wakati wa Fainali za Mataifa ya Barani Ulaya mwaka 2020.
Uwezo wake wa kusakata Kabumbu na kufumania nyavu za timu pinzani uliisaidia Klabu yake (Real Madrid) Kutwaa Ubingwa wa 14 msimu uliopita, huku akitajwa kama Mchezaji Bora Duniani kwa kutwaa tuzo ya Ballon d’Or 2022.