Mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia mwaka 2022 (Ballon d’Or) Karim Benzema huenda akawa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kitakachoikabili Argentina Jumapili (Desemba 18) katika mchezo wa Fainali wa Michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Qatar.
Benzema alitajwa kwenye kikosi cha wachezaji 26 wa Ufaransa, lakini siku moja kabla ya kuanza kwa Fainali hizo aliumia na kuondolewa kikosini, lakini Kocha Mkuu wa ‘Les Bleus’ Didier Deschamps hakuziba pengo lake.
Taarifa zinaeleza kuwa Benzema amepona majeraha yaliyokua yanamsumbua na jana Alhamis (Desemba 12) alikuwa katika kambi ya Ufaransa kabla na baada ya mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya Morocco.
Hata Hivyo alipoulizwa Kocha Mkuu wa Ufaransa Didier Deschamps kuhusu uhakika wa kumtumia Benzema katika mchezo wa Fainali, hakutaka kujibu swali hilo ambalo liliulizwa kwa shauku kubwa na waandishi wa habari, baada ya mchezo dhidi ya Morocco.
“Sipo tayari kujibu swali hilo,” alijibu Didier Deschamps alipohojiwa kuhusu kurejea kwa Benzema.
Hata hivyo pamoja na tetesi hizo kuchukua nafasi kubwa katika vyombo vya habari vilivyokita kambi nchini Qatar, bado Ufaransa itapaswa kujiandaa kwa hali yoyote ile, ili kuikabili Argentina katika mchezo wa Fainali, na kutetea Ubingwa wa Dunia ambao waliutwaa mwaka 2018 katika Fainali zilizounguruma nchini Urusi.
Ufaransa ilianza harakati za kutetea taji hilo mwaka huu ikitokea Kundi D, lililokuwa na timu za Australia, Tunisia na Denmark.
Ufaransa ilianza kupambana na Australia Novemba 22 katika Uwanja wa Al Janoub, mjini Al Wakrah, na kuibuka na ushindi wa 4-1, mabao yakifungwa na Rabiot, Giroud aliyefunga mawili pamoja na Mbappé, huku bao la Socceroos likifungwa na Goodwin.
November 26 Ufaransa ilicheza mchezo wake wa Pili kwa ulishuhudia wakipapatuana na Denmark iliyokubali kufungwa 2-1.
Mabao katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa 974 mjini Doha yalifungwa na Mbappe huku Andreas Christensenj akiifungia Danish Dynamite bao la kufutia machozi.
Ufaransa ilitupa karata yake ya tatu na ya mwisho katika Hatua ya makundi kwa kucheza na wawakilishi wa Afrika Tunisia mnamo November 30 katika uwanja wa Education City uliopo katika mji wa Al Rayyan na kukubali kupoteza kwa kufungwa 1-0, lililofungwana Wahbi Khazri.
Katika hatua ya 16 Bora Ufaransa iliendeleza wimbi la ushindi kwa kuifunga Poland mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Al Thumama mjini Doha mnamo Desemba 04, mabao yakifungwa na Giroud pamoja na Mbappé aliyefunga mawili, huku Gwiji Lewandowski akiifungia The Eagles bao la kufutia machozi.
Ilipotinga hatua ya Robo Fainali Ufaransa ilikutana uso kwa macho na England katika Uwanja wa Al Bayt, mjini Al Khor mnamo Desemba 10, na kuendeleza ubabe kwa kuwabanjua wajukuu wa Malikia Elzibeth mabao 2-1, mabao ya Les Blues yakifungwa na Tchouaméni na Giroud, huku Harry Kane akiifungia The Three Lion bao la kufutia machozi.
Hatua ya Nusu Fainali Ufaransa ikacheza dhidi ya Morocco katika Uwanja wa Al Bayt, mjini Al Khor mnamo Desemba 14 na kuibuka na ushidni wa 2-0, mabao yalifungwa na Théo Bernard François Hernandez pamoja na Kolo Muani.