Vipimo vya afya alivyofanyiwa bondia wa ngumi za kulipwa, Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’, vimeonyesha kuwa yupo fiti na anaweza kupanda ulingoni kuzichapa.
Mandonga alifanyiwa kipimo cha kichwa na utimamu wa mwili mwanzoni mwa juma hili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya kupokea kichapo kikali.
Bondia huyo mwenye umri wa miaka 42 kutoka mkoani Morogoro, alidundwa na Moses Golola kutoka Uganda katika pambano la kimataifa lililofanyika majuma mawili yaliyopita.
Baada kupigwa, Mandonga alifungiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania TPBRC), kutocheza pambano lolote hadi itakapothibitishwa kuwa yupo sawa.
Akizungumza jijini Der es salaam, Daktari wa TPBRC, Khadija Hamisi, amesema majibu ya vipimo alivyofanyiwa Mandonga vimeonyesha kuwa hana tatizo lolote.
Khadija amesema kutokana na ripoti hiyo, bondia huyo anaweza kufanya mazoezi na kupanda ulingoni wakati wowote.
“Ililazimu Mandonga afanyiwe vipimo hasa cha kichwa baada ya uwepo wa tetesi kuwa huenda ana tatizo katika ubongo kutokana na vipigo vya mara kwa mara amabvyo amekuwa akipokea katika mapambano anayocheza, majibu yametoka kuwa yupo sawa na anaweza kuendelea kucheza masumbwi,” amesema Khadija.
Katibu wa TPBRC, George Lukindo, amesema shirikisho limetoa kibali kwa Mandonga kucheza pambano Visiwani Zanzibar.
Amesema pamoja na Mandonga, mabondia watakaopigwa KO au TKO hawaruhusiwi kupanda ulingoni katika muda wa wiki mbili kwani katika kipindi hicho wanapaswa kuwa chini ya uangalizi wa daktari.
Mandonga amesema “Nashukuru Mungu nipo salama, najipanga kwa pambano langu la Zanzibar, mashabiki na wadau wa masumbwi wategemee mambo mazuri kutoka kwangu.”
Mandonga, baba wa watoto sita, anatarajia kupanda ulingoni Agosti 27 mwaka huu kumkabili Muller JR.