Baraza La Vyama Vya Soka Afrika Mashariki Na Kati (CECAFA), limeiondoa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Zanzibar (Karume Boys), kwenye michuano ya vijana inayoendelea mjini Bujumbura nchini Burundi.
CECAFA wamefikia maamuzi ya kuiondoa timu hiyo, baada ya kubaini mapungufu ya baadhi ya wachezaji ambao hawana sifa ya kushiriki michuano hiyo, inayostahili kwa wachezaji walio na umri chini ya miaka 17.
Kanuni ya michuano hiyo kwa mwaka huu, inayataka mataifa shiriki kupeleka wachezaji waliozaliwa kabla ya Januari 1 mwaka 2002, ambao kimahesabu wanakua na umri kamili wa miaka 17 au chini ya hapo.
Hata hivyo mbali na kuiondoa Karume Boys, CECAFA wametangaza kuifungia Zanzibar kushiriki michuano hiyo ya vijana chini ya umri wa miaka 17 kwa muda wa mwaka mmoja, sambamba na kuitoza faini ya dola za Kimarekani 15,000.
Wakati huo huo kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 cha Tanzania bara (Serengeti Boys), jana kilianza michuano hiyo kwa kupata sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Uganda.