Mlinda Lango na Nahodha wa KMC FC Juma Kaseja amesema kikosi chao hakikucheza vizuri dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa Mzunguuko wa 17 wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa jana Jumatatu (Machi 07), Uwanja wa Azam Complex Chamazi Jijini Dar es salaam.

KMC FC ilikua wenyeji wa mchezo huo uliomalizika kwa Coastal Union kuibuka na ushindi wa 3-2, ikitokea nyuma baadaya kuongozwa kwa mabao 2-1.

Kaseja ambaye alikua langoni mwa KMC FC katika mchezo huo, amesema kwa ujumla hawakujituma kwa asilimia zote, hali iliyopelekea kukubali kupoteza alama tatu nyumbani.

Amesema walicheza kwa umakini kwa vipindi tofauti, lakini katika dakika za mwisho, walipoteza umakini na kujikuta wakikubali kuipa Coastal Union nafasi ya kuondoka na furaha ugenini.

“Kwa ujumla hatukucheza vizuri katika mchezo wa jana, tulionekana wadhaifu kwa nyakati fulani, hivyo tulitoa nafasi kwa wapinzani kutuadhibu na kuondoka na alama tatu katika Uwanja wetu wa nyumbani,”

“Tumekubali matokeo ya mchezo huo, ninaamini Benchi la Ufundi limeona wapi tulipokosea na litafanya marekebisho ili tuweze kucheza vizuri katika mchezo wetu unaofuata.” amesema Kaseja

Katika mchezo ujao, KMC FC itacheza dhidi ya Young Africans itakayokua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikikumbuka kichapo cha mabao 2-0, ilichokipokea kutoka kwa wakongwe hao katika mchezo wa Duru la Kwanza uliopigwa Uwanja wa Majimaji Songea mkoani Ruvuma.

KMC FC inashika nafasi ya 06 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 22, huku Coastal Union ya Jijini Tanga iliyoondoka la alama tatu ugenini Jijini Dar es salaam jana Jumatatu (Machi 07) ikifikisha alama 21 zinazoiweka kwenye nafasi ya 10.

https://youtu.be/FqRNnfW89tU

AZAM FC: Unapoanza kuamini, unasahau kushindana
Wanawake 98 waapishwa kuwa Majaji Misri