Mlinda Lango Mkongwe katika Ligi Kuu Tanzania Bara Juma Kaseja amevunja ukimya na kueleza mazingira yanayomzunguuka tangu alipoanza kupata umaarufu katika soka la Bongo.
Juma Kaseja ambaye ni miongoni mwa wachezaji waliobahatika kuzitumikia klabu nguli za Tanzania Simba SC na Young Africans kwa nyakati tofauti, amesema katika kipindi chote cha kulitumikia soka la Bongo hakuwahi kutegemea ushirikina na badala yake anamtegemea Mwenyezi Mungu.
Hata hivyo Kaseja amesema licha ya yeye kutojihusisha na masuala la kishirikina, bado wadau wa michezo nchini wamekua wanamtaja kuwa kinara wa masuala hayo, jambo ambalo amelisikia kwa muda mrefu na kulipuuza.
“Unaweza kufanya kitu na watu wasione, sasa mimi kuna wakati nilikuwa naandika ujumbe kwenye fulana yangu kwamba ‘There Is Only Kaseja (Kuna Kaseja Mmoja Tu)’ kwa hiyo zile jumbe zilikuwa za watu ili waheshimu wenzao kutokana na juhudi wanazoonyesha kwa kuachana na kashfa ambazo hazikuwa na maana,”
“Mpira wetu wa Tanzania una changamoto nyingi kwa upande wangu nimeweza kupambana nazo na kufanikiwa kufika hapa nilipo. Kama ningekuwa mtu wa kukata tamaa nadhani ningekuwa nimeshastaafu soka, halafu ishu ya ushirikina ingekuwa na maana basi mimi ningedakia hadi Barcelona,” amesema Mlinda Lango huyo ambayo kwa sasa anaitumikia KMC FC ya Dar es salaam.
Kaseja pia amewahi kuitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania ‘TAIFA STARS’ kwa nyakati tofauti, huku akiwa miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Simba SC kutinga hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika mwaka 2003, baada ya kuwatoa mabingwa kwa wakati huo Zamalek ya Misri.