Watu 14 wameuawa na wengine 28 kujeruhiwa baada ya Polisi kuwafyatulia risasi wakazi waliokuwa na hasira kutokana na matukio ya utekaji nyara, mauaji na visa vya kikatili ambavyo viomekuwa vikitukia mara kwa mara.
Taarifa ya tukio la vifo hivyo, imetolewa na Mbunge wa Wilaya ya mashariki ya Ikongo nchini Madagascar, Jean Brunelle Razafintsiandraofa na kusema Polisi walifanya kitendo hicho siku ya Jumatatu Agosti 29, 2022.
Amesema, milio ya risasi ilisikika eneo lililokuwa na watu hao wenye hasira, na kwamba kilichotakiwa kufanywa ni kutumia busara za kuwatawanya watu hao na si kuwashambulia kwani walikuwa na hasira ya matukio ya utekaji nyara yanayotukia kwa baadhi ya vipindi.
“Ni hivi juzi tu tumepata mshtuko kwa mashuhudia wa hapa Ikongo kusema mtoto mwenye ualbino alitoweka na mamlaka inashuku utekaji nyara sasa badala ya kutoa majibu au kuchukua hatua rafiki tena Polisi inawashambulia raia wake sasa hii ni nini,” aliuliza Mbunge huyo.
Awali, Daktari Mkuu Wa Hospitali ya Ikongo, Dkt. Tango Oscar Toky alisema, “Watu tisa walikufa papo hapo na kati ya watu 33 waliojeruhiwa waliopokelewa asubuhi, watano walikufa hospitalini na wengi wa majeruhi walifika hapa wakiwa na hali mbaya.”
Katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi, watu wenye ualbino wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili vinavyohusishwa na imani za kishirikina, uwepo wa matukio zaidi ya dazeni ya utekaji nyara, mashambulizi ya kutisha na mauaji.
Licha ya juhudi za Polisi za kuwakamata watu wanne ambao ni washukiwa wa matukio tofauti lakini vitendo hivyo, vimewafanya raia kuazimia kujichukulia haki mikononi na kufika kambi ya gendarmerie kuomba wakabidhiwe watuhumiwa hao wanne.