Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameonesha kutoridhishwa na kasi ya Ujenzi wa Mabweni ya Shule ya Sekondari Mazae na kuwataka kujipanga vizuri kwa hatua zote kwani muda uliosalia wa kidato cha tano kuwasili shuleni hapo umekaribia.
Senyamule ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Mpwapwa kukagua miradi na miundombinu inayojengwa katika Shule hiyo na kuwataka wahusika kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wajipange na vifaa visivyokuwepo vinunuliwe.
“Kwenye upande wa Madarasa niwapongeze, Ila mabweni lazima siku zilizobaki tujipange vizuri na tuhakikishe yanakamilika kwa wakati, wapo watoto watakao toka Mikoa mbalimbali watahitaji kukaa bweni hakikisheni mnayamaliza,” amesema Senyamule.
Aidha ameongeza kuwa, “sasa zimebaki wiki mbili tuone hamlali usingizi mfanye kazi nyingi kwa wakati mmoja, ili tusimwangushe Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini ambacho hakijanifurahisha zaidi mnaleta vifaa nusu nusu zingatieni maelekezo tunayotoa kama Mkoa, Mjipange vifaa ambavyo
havipo hakikisheni mnavinunua.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpwapwa, George Fuime ameahidi kuyasimamia kikamilifu maagizo yaliyotolewa na Mhe. Senyamule kwa kuongeza nguvu kazi na kupanga mpango Mkakati utakaowasaidia kukamisha miradi hiyo kwa wakati.