Kuna kila dalili kwamba huenda kasi ya Rais John Magufuli haitaacha ‘jiwe juu ya jiwe’ katika eneo ambalo linamilikiwa kinyume cha sheria, na huenda vilio vya wanyonge na wenye nacho vikafanana.

Serikali imeteua timu ya maafisa ardhi kuchunguza uhalali wa umiliki wa eneo la kiwanja namba 719/3 lililopo Mikocheni mtaa wa TPDC linalomilikiwa na Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye baada ya kudaiwa kuwa ni eneo la wazi lililovamiwa.

Inadaiwa kuwa Sumaye alilivamia eneo hilo ambalo miaka ya 1970 lilikuwa eneo la wazi lililokuwa likitumika kwa ajili ya michezo na mikutano ya siasa na mikusanyiko mingine.

Mbali na Sumaye, wengine waliodaiwa kulivamia eneo hilo na kufanya ujenzi ni pamoja na mfanyabiashara mkubwa ambaye ni mmiliki wa Maduka ya S.H Amon  na Mbunge wa jimbo la Rungwe, Saul Amon. Mwingine aliyetajwa ni Katibu Mkuu Mstaafu, Ofisi ya Rais, Philemon Luhanjo.

Wiki tatu zilizopita, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa TPDC alifika katika eneo hilo akiwa na maafisa ardhi wa Wilaya ya Kinondoni na kutoa notisi ya ‘mdomo’ ya kusitishwa kwa shughuli za ujenzi zilizokuwa zinaendelea katika eneo hilo. Alieleza kuwa ujenzi unaoendelea haufuati sheria kwa kuwa hakuna kibao cha kandarasi kilichowekwa kuonesha shughuli ya ujenzi iliyokuwa ikiendelea.

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema kuwa ifikapo Jumatatu ya wiki ijayo, serikali itavunja uzio wa eneo hilo na kusitisha rasmi shughuli za ujenzi endapo ripoti ya uchunguzi unaoendelea itabaini uvunjivu wa sheria.

 

Rais Amuokoa Mwanaume Aliyetaka Kujiua kwa Kujirusha Kutoka Darajani
Lowassa aanza Kuchunga Ng’ombe, Atoa Neno kwa Watanzania