Serikali nchini imedhamiria kufanya maboresho katika sekta ya Elimu yenye lengo la kuhakikisha mahitaji ya watanzania yanaendana na kasi ya utandawazi na mabadiliko ya kiteknolojia.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo Juni 8, 2022 katika kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa idara ya udhibiti wa ubora wa shule kilichofanyika ukumbi wa vijana Jijini Dodoma.

“Maboresho katika sekta ya Elimu ya lengo la kuhakikisha mahitaji ya watanzania yanaendana na kasi ya utandawazi na hii itasaidia kuchangamkia fursa ikiwemo ufundishaji wa Kiswahili kwa vyuo vya nje,” amesema Mkenda.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa malezi kwa watoto shuleni ambao hawakai muda mwingi na wazazi wao ambao huhitaji uangalizi katika ukuaji wao wa kielimu, tabia na maisha kiujumla.

“Hili liangaliwe sana maana tunaona kwenye mitandao mambo ya hovyo yanatokea na tusingependa kupuuza tutakuja na tamko na mikakati baada ya kupitia vipengele mbalimbali,” alisisitiza Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa, uboreshaji huo wa elimu kwa kupitia sera ya elimu ya mwaka 2014 na mapitio ya mitaala, ni ajenda ya serikali kupitia maelekezo ya Rais Samia aliyoyatoa wakati akilihutubia Bunge la 12  Aprili 22, 2021.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji Prof. James Mdoe alimpongeza Waziri Mkenda kwa kuwathamini wadhibiti ubora kwa kuhudhuria katika mkutano huo na kuwaongezea nguvu ya ufanisi wa kazi.

Kikao hicho cha siku tatu kilichoanza Juni 7, 2022 kimewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa uthibiti ubora wa shule makao makuu, wadhibiti ithibati ya shule na wadhibiti ubora wa shule wakuu wa kanda na wilaya na kinatarajia kumalizika rasmi Juni 9, 2022.

Young Africans yatuma ujumbe Tanga, yatamba kuibanjua Coastal Union
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Juni 09, 2022