Maagizo ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibari, Dkt. Ali Mohamed Shein yameanza kutekelezwa kwa vitendo mkoani Kaskazini Pemba kwa kugawa majukumu ya utekelezaji wa maagizo hayo kwa maofisa Wadhamini wa Wizara na taasisi za Serikali Kisiwani Pemba.
Hayo yamebainishwa na mkuu wa mkoa huo, Omar Khamis Othman wakatia akizungumza katika kikao cha kutathmini ziara ya Rais Shein, ambapo amewataka wakuu wa Idara za Serikali kuwa wakweli na wawazi ili kuendana na kasi ya utendaji wa Rais huyo kwa kuhakikisha maagizo hayo wanayafanyia kazi .
Amesema kila Wizara inapaswa kushiriki katika kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo yaliyotolewa na Rais wakati wa ziara yake mwezi uliopita katika Mkoa huo.
“ Ni vyema kila mmoja anatakiwa kuwajibika kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Rais Shein aliyoyatoa wakati wa ziara yake katika Mkoa wetu , hii itasaidia kwenda kasi na Rais wetu ”alieleza.
Maofisa wadhamini wameeleza kuwa tayari wameanza kuyafanyia kazi maagizo ya Rais kwa kufanya ziara na mikutano ya watendaji wa taasisi zao.
Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Kaskazini Pemba, Ahmed Khalid Abdalla amewapongeza maofisa wadhamini kutokana na mchango wao uliofanikisha ziara ya Rais katika mkoa huo .
Na kwaupande wake Mkuu wa Wilaya ya Wete, Rashid Hadid Rashid amewasisitiza wakuu hao wa taasisi kuhakikisha wanawajibika katika kutekeleza maagizo ya Rais kwa uwazi ili wananchi wazidishe imani na serikali yao.