Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Simba SC Kassim Dewji amefichua ukweli wa mambo ndani ya klabu hiyo, baada ya kushindwa kutetea mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Kassim Dewji ambaye ni kiongozi Mwandamizi ndani ya Simba SC, amefichua ukweli huo katika mahojiano maalum na Kituo cha Radio cha EFM leo Jumanne (Mei 30) jijini Dar es salaam.
Kassim amesema ukongwe wa wachezaji na kukosa hamu ya kusaka mafanikio zaidi ndani ya kikosi cha Simba SC ndio chanzo cha klabu hiyo kufanya vibaya msimu huu 2021/22.
“Imefikia wakati wachezaji tulionao hawana hamu ya kupambana kwa hamu ya kusaka mataji ya ndani, kama Ligi Kuu na ASFC wameshachukua zaidi ya mara moja, kwa hiyo waliona hakuna kipya kwao, “
“Hata upande wa Kimataifa wachezaji wetu walionyesha kupambana na kwa hilo tunawapongeza, lakini kama kufika Robo Fainali wamefika zaidi ya mara moja, hivyo kwa mtazamo wangu uwezo wao ndio uliishia pale.” amesema Dewji
Simba SC imepoteza ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne, pia imepoteza ASFC kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili.