Barabara inayounganisha mikoa ya Katavi na Tabora ambayo pia hutumika kusafilishia abiria na chakula kwenda mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa ya kaskazini na kati, imefungwa.
Barabara hiyo imefungwa jana baada ya daraja la mto koga linalounganisha mikoa hiyo miwili kujaa maji na kuhatarisha usalama wa watu na vyombo vya usafiri.
Uamuzi wa kufunga barabara hiyo ulitolewa jana na kaimu mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya ya Mpanda, Liliani Matiga baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa katavi na uongozi wa wilaya ya Mlele kufika kwenye eneo hilo na kushuhudia maji yakiwa yamejaa na kupita juu ya daraja kwa kasi.
Wakati viongozi hao wakiwa katika eneo hilo, magari ya mizigo, magari madogo na ya abiria yalikuwa pembeni baada ya kushindwa kuvuka kutokana na wingi wa maji.
Mhandisi mshauri wa kampuni ya china Wu Yi Contoctins, Stephen Ntibihira amabayo inanedelea na ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kutoka Katavi kwenda Tabora amesema wamepata changamoto ya mto koga kuongezeka maji yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kaimu meneja wa wakala wa barabara Tanzania (Tanroads) , Mkoa wa Katavi, Martin Mwakabende amesema kuwa kutokana na kufungwa kwa barabara hiyo, magari ya abiria na magari ya mizigo kwa sasa yatatumia njia mbadala inayopitia wilayani Uvinza mkoani Kigoma.