Serikali Wilayani ya Tanganyika Mkoani Katavi, imeanza maandalizi ya sherehe za maonesho ya wakulima (nane nane), kwa mwaka 2024.
Hatua hiyo imefikiwa katika kikao cha maendeleo ya wilaya ya Tanganyika kilichofanyika Novemba 8, 2023 katika ukumbi wa Mkurugenzi wilayani humo, huku Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu akiagiza kuundwa kwa kamati maalumu itakayoratibu mchakato wa maandalizi hayo ndani ya siku 10.
Kwa mujibu wa Afisa kilimo wa wilaya ya Tanganyika, Philemoni Mwita amesema maonesho hayo yatasaidia kuwafikia wakulima wengi zaidi katika wilaya ya Tanganyika na mkoa wa Katavi badala ya kutegemea maonesho ya kikanda yanayofanyika mkoa wa Mbeya.
Kwa miaka mingi sasa mkoa wa Katavi umekuwa ukisafirisha wakulima kwenda kushiriki maonesho ya nane nane katika mkoa wa Mbeya hali ambayo DC Buswelu ameeleza imekuwa ikiigharimu serikali fedha nyingi huku ikiwanyima fursa wakulima wengine kunufaika na sherehe hizo.