Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema amesikitishwa na tukio lililotokea Oktoba Mosi, 2022 katika uwanja wa mpira wa miguu huko Malang nchini Indonesia, ambapo zaidi ya watu 174 waliripotiwa kufariki kutokana na ghasia baada ya kumalizika kwa mchezo wa mpira.
Kwa mujibu wa taarifa, iliyotolewa na Msemaji wa Katibu Mkuu, Stephane Dujarric jijini New York nchini Marekani imesema kuwa Guterres, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na amewatakia majeruhi ahueni ya haraka.
Amesema, “Katibu Mkuu anazitaka mamlaka husika kufanya uchunguzi wa haraka na wa kina juu ya tukio hili na kuchukua hatua zote zinazohitajika, ili kuepusha kujirudia kwa janga hilo.”
Takriban watu 174 walifariki, na wengine zaidi ya 180 kujeruhiwa katika uwanja wa mpira wa miguu nchini Indonesia, baada ya maelfu ya mashabiki wa waliokuwa na hasira kuvamia uwanja na Polisi kuwarushia mabomu ya machozi hali ambayo ilisababisha kuanguka na kukanyagana.
Tukio hilo, lilitokea usiku wa Jumamosi Octoba 1, 2022 katika mji wa Malang, nchini Indonesia kufuatia mashabiki hao kupandwa na hasira baada ya timu yao ya Arema FC kufungwa 3-2 na timu pinzani ya Persebaya Surabaya kwenye uwanja wa Kanjuruhan.
Polisi nchini humo, ambao walilitaja tukio hilo kama machafuko, walijaribu kuwashawishi mashabiki kurudi kwenye maeneo yao ya kuketi lakini haikuwezekana na hivyo kutumia vitoa machozi baada ya wenzao wawili ambao ni maafisa Polisi kuuawa na magari yao kuharibiwa.