Jumuiya ya Afrika Mashariki inatarajia kumpata katibu Mkuu wake mpya mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao Jumamosi ya Februari 27,2021.
Hayo yamebainika katika Mkutano wa 40 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kupitia ajenda mbalimbali za kuwakilisha katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa kawaida wa 21 sambamba na kupitia nyaraka muhimu kuhusu maendeleo ya jumuiya hiyo huku mambo muhimu ambayo wakuu hao wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watakayoyajadili watakapokutana yakitajwa.
Aidha, Prof. Kabudi ameongeza kuwa mbali na uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya hiyo pia kutakuwepo na uteuzi wa majaji watatu wa chemba ya rufaa ya mahakama ya haki ya Afrika Mashariki pia majaji wengine wa chemba ya mahakama ya mwanzo ya Jumuiya hiyo halikadhalika uteuzi wa Rais Jaji na makamu wake wa mahakama ya haki akiwemo Jaji Kiongozi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Awali,Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulitanguliwa na Mkutano wa Maafisa Waandamizi wa jumuiya hiyo ambapo Katibu mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi,Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameanisha masuala anuai ambayo Jumuiya ya Afrika Mashariki katika utengamano huo wanahitaji kuendelea kuyasukuma mbele ili jumuiya hiyo iwe na tija kwa wananchi wake.
Mkutano wa kawaida wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utafanyika kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao kutokana na uwepo wa ugonjwa wa COVID – 19 ambapo Rwanda imeiongoza Jumuiya hiyo kwa muda wa miaka miwili sasa.