Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amemuapisha Mhandisi Zena Ahmed Said, kuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, akichukua nafasi ya Dkt. Abdulhamid Yahya mzee aliyestaafu.
Hafla hiyo ya kiapo imefanyika Ikulu Jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Mawaziri, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid.
Rais Dkt. Mwinyi amemuapisha kiongozi huyo kushika wadhifa huo baada ya kumteua Januari mosi mwaka huu, kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 49 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Zena Ahmed Said alikuwa Katibu mkuu Wizara ya Nishati katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na vyombo vya habari, Zena amesema atajitahidi kufanya kazi zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliopo ili kufikia matarajio ya Wazanzibari na kujiongeza katika ubunifu ili aweze kufikia malengo, huku akiahidi Serikali kuangalia kwa undani umuhimu wa ajira kwa vijana.
Aidha, ametoa wito kwa wanawake nchini kote kujiamini na kufanya kazi zao kwa weledi pamoja na kuwataka kufanya shughuli zao kwa kuzingatia wakati na nafasi zao, sambamba na kutosubiri kusaidiwa.
Mhandisi Zena Ahmed Said, anakuwa mwanamke wa kwanza nchini kushika wadhifa wa Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, tangu Mapinduzi ya 1964.