Katibu wa Siasa na Uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe Erasto Ngole, amewataka wanafunzi wa vyuo, vyuo vikuu pamoja na vijana kujitafutia mabadiliko na maendeleo badala ya kuisubili serikali iwafanyie kila kitu.
Ameyasema hayo alipokutana na wanafunzi wa vyuo kupitia idara ya vyuo na vyuo vikuu chini ya umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi CCM mkoani humo waliokutana mjini Njombe kwa lengo la kuimarisha uhai wa Chama hicho.
“Mabadiliko na maendeleo yako yanaanza na wewe, hakuna serikali duniani ambayo iliwahi kuamka na kuwagawia watu wake wote fedha hakuna,ukiona wewe kwa siku unachomoa elfu tano ukaitumia lakini mwili unakutaka ili uridhike huduma ya shilingi elfu kumi unatakiwa uichukie hiyo hali na uchukue hatua,”amesema Ngole
Amesema kuwa mtaji unatafutwa kwa namna yoyote hivyo ni vyema vijana kusoma mazingira na kwenda kutafuta mitaji na kuilinda kuliko kuwa na wasomi wengi wanaoshindwa kutumia elimu zao.
Aidha, amewataka wanawake kutumia uwezo wao kupiga hatua kimaendeleo kama ilivyo kwa baadhi ya wanawake waliofanikiwa nchini kuliko kusubili wanaume.
“Akina dada mimi naomba niwajengee ujasili, Mungu aliwaumba kwa makusudi akawapa utashi ndio maana kuna wakina Samia na wakina Tulia Ackson bado kuna wafanyabiashara wakubwa wengi tu, acheni kuwa na fikra ya kuolewa tu, wapo wanaume wajinga wajinga ninyi tafuteni pesa kama kuna wanaume wajinga oeni na wafuate masharti yenu, sina nia mbaya ila nataka wote tujiongeze,”ameongeza Ngole
Hata hivyo, nao baadhi ya vijana waliohudhulia katika mkutano huo wameshukuru namna walivyopewa elimu ya kujitambua huku wakiahidi mabadiliko pindi wawapo katika jamii.