Mfanyabiashara maarufu na Kiongozi wa upinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC, Moise Katumbi amewasilisha ombi la kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi Mkuu wa Taifa hilo unaotarajia kufanyika Desemba 2023.
Katumbi ambaye pia ni tajiri mkubwa na Gavana wa zamani wa mkoa wa Katanga sasa ataingia katika ushindani na Rais wa Taifa hilo, Felix Tshisekedi na Martin Fayulu ambaye alikuwa mshindi wa pili katika uchaguzi uliopita na mshindi wa Tuzo ya Nobel ya magonjwa ya Wanawake, Denis Mukwege.
Hata hivyo, Mpinzani wake Rais Tshisekedi qmbaye ni mtoto wa Kiongozi wa upinzani wa muda mrefu wa DRC, Etienne Tshisekedi muhula wa kwanza katika utawala wake amekumbwa na msukosuko ya matatizo ya kiuchumi, milipuko ya magonjwa na kuongezeka kwa mashambulizi ya wanamgambo katika eneo la Mashariki.
Aidha, Chama chake cha Ensemble pour la Republique pia kinatarajia kutangaza mpango wake ambao unalenga kurejesha usalama, kutengeneza ajira na kuboresha huduma za kijamii lakini hiyo haitafanya kupunguza ushindani wa Katumbi ambaye ana wafuasi wa kutosha ndani ya Taifa hilo.