Klabu ya Mtibwa Sugar iko kwenye hatua za mwisho za kumuajiri aliyekuwa Kocha Mkuu wa Ihefu, Zubery Katwila kwa ajili ya kukinoa kikosi hicho, huku uongozi ukisema walioomba wamefikia watano.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo zinaeleza kuwa, taratibu za kutafuta kocha mkuu zimeanza na muda wowote wataweka wazi atakayechukua mikoba ya Habibu Kondo aliyetimuliwa kutokana na matokeo mabaya.
“Mchakato huo umeanza mara moja na viongozi vanalifanyia kazi kwa haraka, lengo ni kuona tunapata mtu sahihi ambaye kwa pamoja tunaamini atatutoa hapa tulipo na kutupeleka mbele zaidi ya tulivyoanza msimu huu,” kilisema chanzo chetu.
Kwa upande wa ofisa habari na mawasiliano wa klabu hiyo, Thobias Kifaru amesema wapo zaidi ya makocha watano walioomba kazi ingawaje bado hawezi kuwaweka wazi kwa sasa hadi pale makubaliano baina ya viongozi na wao yatakapokamilika rasmi.
“Siwezi kusema Katwila yupo kwenye mchakato au hayupo kwa sababu bado mazungumzo yanaendelea, kikubwa sisi tumeelekeza nguvu zaidi katika mchezo wetu wa jana dhidi ya Kagera Sugar na baada ya hapo ndipo tutaweka wazi,” amesema.
Wakati Kifaru akizungumza hayo, imefahamika kuwa Katwila anapewa nafasi kubwa ya kuiongoza timu hiyo kutokana na ushirikiano alionao baina yake, viongozi na wachezaji huku wakiamini ni kocha sahihi atakayewaletea matokeo chanya.
Katwila anaenda kuifundisha timu hiyo ikiwa ni siku chache tu tangu atimuliwe Ihefu na Mganda, Moses Basena kuchukua mikoba yake.