Padri mmoja nchini Marekani amejiuzulu utumishi wake wa upadri aliotumikia kwa miaka mingi baada ya kufahamika kuwa amekuwa akiwabatiza watoto kwa kauli tata ambayo imebatilishwa na viongozi wa kanisa la Roma kutoka Italia.
Padri huyo, Andres Arango, ambaye amesemekana kuwa alibatiza maelfu ya watoto kwa miaka mingi na kwa maeneo tofauti amekuwa akitumia kauli ya ‘Tunawabatiza’ badala ya ‘Ninakubatiza’
Katika barua ambayo iliandikwa na mkuu wa dayosisi ya Phoenix huko Marekani, Askofu, Thomas J. Olmsted, ilisema “Ni katika unyenyekevu wa mashauri ya kidini ninawaarifu kuwa batizo ambazo zimefanywa na mchungaji Arango kwa miaka kadhaa ni batili kwa sababu amekuwa akikosea matamshi yanayotakiwa katika ubatizaji.”
“Maamuzi haya yanakuja baada ya utafiti uliofanywa na kusanyiko la viongozi wa mafundisho ya imani huko Roma Italia, Arango amekuwa akisema ‘Tunakubatiza katika jina la baba, mwana na roho mtakatifu’ badala ya ‘Ninakubatiza kwa jina la Baba, mwana na Roho mtakatifu,” ilisema barua hiyo.
Askofu Olmsted aliongeza kuwa katika sentensi hiyo kosa kubwa hapo ni kuwa anayebatiza ni Yesu Kristo kupitia kwa Padri huyo na sio jamii nzima inayohusika kumpatia mtu sakramenti hiyo takatifu na hivyo mkusanyiko huo wa imani ambao umefanyika mjini Vatican umesema kuwa batizo zote zimekuwa ni batili.
Kwa mujibu wa msemaji wa dayosisi ya Phoenix Burke, ambaye aliongea na shirika la habari ya NBC amesema, Arango amekuwa Padri na amekuwa akibatiza watoto kuanzia mwaka 1995 , ambapo pia amekuwa akifanya shughuli hizo San Diego na Brazili.
Msemaji huyo alisema kuwa kwa miaka yote hiyo hakuna idadi kamili ambayo imetolewa ya walioathirika na ubatizo huo batili ingawa mara ya mwisho Arango alibatiza Juni 17 2021 na inasemekana ni maelfu ya watoto na watu wazima.
Katika barua yake kwenda kwenye parokia aliyoitumikia, padri Arango ameandika “Imenisikitisha kuwa katika utumishi wangu wote nimekuwa nikibatiza watoto kwa ubatili nikitumia kanuni batili, ingawa haikua kusudio langu kuwaumiza watu wengi, ninaomba radhi kwa jamii iliyoathirika na watu wote ambao wao katika parokia nzima niliyokuwa nikutumikia,” alisema Padri Arango.
“Kwa unyenyekevu ninaomba radhi kwa matendo yangu na ninaomba sala zenu katika hili ili nisamehewe na pia naomba mnielewe kuwa sikua nimepanga kufanya hivyo,” aliandika.
Alijiuzulu rasmi Februari 1, 2022, na kuongeza kuwa kwa sasa atatumikia muda wake kuhakikisha kuwa madhara yaliyotokea yanapunguzwa na kuponya wale walioathirika na hata hivyo dayosisi imesema kuwa utumishi wake utaendelea kama mtumishi mwema aatakaefanya matendo mengine ya imani.
Hata hivyo watu wote ambao wanafahamu kuwa walibatizwa na padri huyo kwa miaka hiyo tajwa wametakiwa kujaza fomu maalumu ambazo zimetolewa mtandaoni hata wote ambao wamepewa sakramenti ya ndoa wanatakiwa kurudia viapo vyao ili wawe katika njia njema ya imani.