Mshambuliaji Cristiano Ronaldo amesema hajutii kauli aliyoitoa mjini Kiev, Ukerain mara baada ya klabu yake kutwaa ubingwa wa barani Ulaya usiku wa jumamosi, kwa kuifunga Liverpool mabao matatu kwa moja.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Ureno alihojiwa na mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha BeIN Sports kwa lugha ya kispaniola na kusema “Nitatangaza mustakabali wangu siku chache zijazo “.
Ronaldo pia akauzngumzia muda wake wa kuendelea kuwepo Santiago Bernabeu baada ya kuulizwa swali hilo, na alijibu kwa kusema “Ulikua wakati mzuri nikiwa Real Madrid.”
Kauli hizo mbili zimepokelewa tofauti na mashabiki wa Ronaldo pamoja na Real Madrid na kuzua hofu, huenda mshambuliaji huyo akawa mbioni kuondoka baada ya kutwaa ubingwa wa Ulaya mara nne akiwa klabuni hapo.
Alipoulizwa baadae kama kauli hizo alizitoa kutokana na furaha iliyokua moyoni mwake baada ya kufikisha taji la nne la Ulaya akiwa na Real Madrid, Ronaldo alijibu “Nilizungumza nikiwa na maana kubwa, sikusema eti kwa sababu nilikua na furaha iliyopitiliza, kikubwa mashabiki wanapaswa kusubiri na kuona nini kinachofuata.”
“Muda si mrefu nitafanya jambo ninalolikusudia kwa vitendo, ninawasihi tena mashabiki, waendelee kuwa na subra wala wasiwe na pupa ya kutaka kujua nilimaanisha nini kwa kauli zile.
Mbali na kutwaa ubingwa wa Ulaya mara nne akiwa na Real Madrid, Ronaldo amefikisha taji la tano la michuano hiyo tangu alipoanza kucheza soka la ushindani barani humo, moja akilichukua akiwa na klabu yake ya zamani ya Man Utd.