Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi wamejitokeza kwa mara ya kwanza kwa kuingilia kati sakata la Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof Mussa Assad na Spika Job Ndugai kwa kumpongeza CAG kuitikia wito wa Spika.
Wabunge hao wa CCM ni mara ya kwanza kutoa msimamo wao tangu sakata hilo lilipoanza ambapo wamedai maamuzi ya Profesa Mussa Assad yameonyesha ni kuheshimu utawala wa kisheria kwa kiongozi wa mkuu wa Bunge.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa CCM, Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda amesema kuwa wanampongeza sana CAG kwa kuitikia wito wa kamati licha ya kuwepo kwa propaganda za kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya wabunge wa upinzani.
“Tunamshukuru kwa kuheshimu mamlaka ya Bunge, sisi kama wabunge tunadhani hatua ya CAG itasaidia kurudisha mahusiano ya Bunge na ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.”amesema Mapunda
Hata hivyo, Januari 21, 2019 Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali CAG ametakiwa kufika kwenye kamati ya maadili ya Bunge ili kujibu madai juu ya kauli aliyoitoa kuwa Bunge ni dhaifu.