Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima amesema kauli ya hayati Dkt John Magufuli kuhusu chanjo inapotoshwa kwani hakusema watu wasichanje ila kuwe na umakini kutokimbilia chanjo bila kujiridhisha.
Ameyasema hayo leo Jumatano Julai 29, 2021 wakati wa hafla ya uzinduzi wa chanjo ya Covid-19 inayofanywa na Rais Samia Suluh Hassan, Ikulu Dar es Salaam.
Waziri Gwajima amenukuu maneno ya Hayati Magufuli amesema Mnamo Januari 27, 2021 wilayani Chato Hayati Magufuli alisema Wizara ya Afya isiwe inakimbiliakimbilia machanjo bila yenyewe kujidhihirisha.
“Hiki ndicho alichokisema haya Magufuli, wametokea sasa wataalam wakuhariri hii hotuba na kujikita kwenye hicho kivuli na kupotosha”.amesema Waziri Gwajima.
“Halafu wametokea wasikilizaji wanaosikiliza hicho kitu kikishapelekwa wanaenda nacho kuwapotosha wengine, ndugu zangu Watanzania hili jambo sio zuri, ndugu zangu wanahabari hili jambo sio zuri, hotuba za viongozi ni za kuziheshimu ni za kuzichukua kama zilivyo ziende, wananchi waamue wenyewe”.amesema Waziri Gwajima.
“Kwa hiyo leo nakemea upotoshaji huu unaofanywa na nikushukuru Rais kwa kusimama bila kutetereka bila kukatishwa tamaa kuiendeleza kazi hii na kutufikisha hapa siku ya leo,”amesema Waziri Gwajima.