Jeshi la Polisi nchini, limetolea ufafanuzi wa kauli ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana aliyoyatoa Julai 27, 2023 akiwa Bariadi Mkoa wa Simiyu, kwamba hakusema bodaboda wapakie abiria zaidi ya mmoja bali alitumia neno ‘wataenda kushauri’.
Kauli hiyo, inafuatia uwepo wa maswali ya Wanahabari na Wananchi wa kada mbalimbali kwa Jeshi la Polisi, ambapo Msemaji wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP. David Misime amesema watu wote wanaopiga simu wanataka kujua nini msimamo wa Jeshi la Polisi.
Amesema, “matamshi ya Kinana yalisema watazungumza na kuishauri Serikali kupitisha sheria Bodaboda wabebe watu zaidi ya mmoja, na kimsingi Jeshi la Polisi ni wasimamizi wa sheria na miongoni mwa sheria hizo ni kifungu namba 59 cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura 168, ambacho kinakataza pikipiki kubeba abiria zaidi ya mmoja.
Aidha Misime amesema Polisi inawaelekeza bodaboda kufuata sheria ya sasa yenye katazo hilo, na endapo ushauri utakaotolewa utakubalika kisheria na kubadilishwa, basi wataisimamia na waendelee kutopakia abiria zaidi ya mmoja iendelee kufuatwa na kuzingatiwa.