Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kauli ya Hayati John Pombe Magufuli kuwa chini ya tani moja ya mazao yanapoasafirishwa yasitozwe tozo isipokuwa ielekezwe katika mazao yanayozidi tani moja haijafutwa na itaendelea kama ilivyo.
Rais Samia ameyasema hayo hii leo Mei 19, 2022 kupitia hotuba yake aliyoitoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mkoani Tabora na kusisitiza ufuatiliaji ili kuwabaini wale wote wanaoenenda kinyume.
“Kuna kauli iliyotolewa na Rais mpendwa wetu Dr. John Pombe Magufuli kwamba chini ya tani moja ya mazao yanapoasafirishwa yasitozwe tozo bali tozo ziende kwenye mazao yanayozidi Tani moja, hiyo ilikuwa ni kauli ya Rais na Rais hajafuta kwahiyo jambo hilo linasimama kama lilivyo,” amesisitiza Rais Samia.
Kufuatia kauli hiyo Rais amewataka wakuu wa Wilaya na wakurugenzi kusimamia jambo hilo ili lisiende tofauti kwa baadhi ya watu kujineemesha isivyo halali na kupoteza mapato ya halmashauri huku wakitumia njia zisizo na haki.
“Wakuu wa Wilaya na wakurugenzi mkasimamie haya kwasababu inawezekana kabisa Migambo wenu huko wanakwenda kutoza tozo hakuna risiti wala mapato hayaingii kwenye maeneo yenu naomba mkayasimamie hayo,” amesema Rais.
Katika hatua nyingine Rais Samia amewataka Mawaziri kujibidiisha katika kazi na kuepuka maneno na kwamba wanatakiwa kutambua wengi wao ni Vijana hivyo watumie nguvu kazi waliyonayo kufanya kazi kwa ufanisi ili kuletea maendeleo ya nchi.
“Kunaweza kukawa kuna maneno mengi sana lakini hampati maneno kama ninayoyapata Mimi Kiongozi wenu lakini hayanivunji moyo najenga nchi nanyi nataka mjenge nchi chapeni kazi vijana wangu kwa maendeleo ya nchi,” amewatia moyo Mawaziri Rais Samia.
Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa na ziara ya kikazi kwa siku tatu Mkoani Tabora iliyoanza rasmi Mei 17, 2022.