Israel imesema inaweza isishirikiane na serikali ya Rais wa Marekani Joe Biden, kuhusu mkakati wa mpango wa nyuklia wa Iran, iwapo kiongozi huyo atarejea kwenye Mkataba wa Nyukulia wa mwaka 2015 na Iran.
Hayo yameelezwa na mjumbe wa Israel mjini Washington, Balozi Gilad Erdan wakati akizungumza na kituo cha redio cha jeshi la Israel.
Kauli hiyo kuhusu Iran inaonekana kusababisha wakati mgumu kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa kuwa inatolewa wakati ambapo bado kiongozi huyo hajawasiliana moja kwa moja na Biden.
Utawala mpya wa Marekani umesema unataka kuirejesha nchi hiyo kwenye Mkataba wa Nyuklia ambao rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump, alijiondoa na kuweka vikwazo vipya kwa Iran, kama Iran itajizatiti tena kutekeleza masharti iliyopewa.
Erdan amesema Israel haitokuwa sehemu ya mchakato huo iwapo Biden atarejea kwenye makubaliano hayo.