Aliyekua Kocha Mkuu wa Klabu ya Township Rollers ya Botswana, Nikola Kavazovic, anatajwa kuwa chaguo la viongozi wa Young Africans, katika harakati za kujaza nafasi ya Mkuu wa Benchi la ufundi klabuni hapo.

Young Africans ipo kwenye mchakato huo, baada ya kufikia maamuzi ya kumtimua Kocha kutoka nchini Burundi Cedric Kaze sambamba na wasaidizi wake, saa chache baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita jijini Arusha.

Katika mchezo huo Young Africans waliambulia matokeo ya sare ya 1-1, huku wakitangulia kupitia kwa bao lilifungwa na mshambuliajji kutoka nchini Burundi Fiston Abdulrazaq na Polisi Tanzania wakasawazisha kupitia kwa Paul Buswita dakika za lala salama.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Young Africans, Kocha Kavazovic ambaye ni raia wa Serbia, muda wowote anatarajiwa kutua ndani ya klabu hiyo, kufutia wasifu (CV) wake kuwavutia viongozi na kuonekana anafaa.

 “Baada ya kikao cha haraka cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika juzi usiku, kimefikia muafaka wa kumleta kocha huyo, mipango yote imefanyika kutokana na hali ya timu ambapo uongozi umepanga kutumia mapumziko haya kuirekebisha timu kwa kuipatia michezo mingi ya kirafiki.

“Kavazovic atakuja kuungana na kocha msaidizi mzawa ambaye tayari tumeshamtambulisha baada ya kufanya naye mazungumzo,” kimesema chanzo hicho.

Timu alizowahi kuzifundisha kocha huyo ni BASK (1996–2005), OFK Žarkovo (2006–2008), Borac (2008–2010), Resnik (2010–2012), FC Istiklol (2012–2013), Tajikistan (2012–2013), Sri Lanka (2014–2015), New Radiant (2015), Lanexang United (2016), New Radiant (2016), Saif (2016–2017), Township Rollers (2017–2018), AFC Leopards (2018), na Free State Stars (2018–2019).

Kikosi cha Young Africans kwa sasa kipo chini ya kocha wa muda Juma Mwambusi, ambaye alingazwa kushika nafasi hiyo Jumanne (Machi 09) siku mbili baada ya benchi la ufundi kuvunjwa.

TCRA yatakiwa kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa umma
Wanafunzi wengine watekwa Nigeria