Kocha mkuu wa Young Africans Cedric Kaze amesema kikosi chake kipo tayari kwa mshike mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao utaendelea mwishoni mwa juma hili.
Young Africans na klabu nyingine za Ligi Kuu, zitaendelea na harakati za kusaka alama tatu muhimu za ligi hiyo, baada ya kusimama tangu mwishoni mwa mwaka jana, kupisha Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ zilizofikia tamati jana Jumapili kwa Morocco kutetea taji huko nchini Cameroon.
Kocha Kaze amesema wachezaji wake wapo tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mbeya City, ambao utachezwa Jumamosi (Februari 13), Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema kila mchezo kwao ni fainali na wanatambua kwamba wapinzani wao wamejipanga kupata ushindi jambo ambalo halimpi tabu.
“Kila mchezaji anajua majukumu yake akiwa ndani ya uwanja, nina waamini vijana wangu wanafanya kazi vizuri wakiwa ndani ya uwanja hivyo ni muhimu kwetu kushinda.
“Jambo zuri ni kwamba hakuna ambaye anajua nini kitatokea kesho sisi tunaangalia maandalizi yetu pamoja na nguvu kubwa kwenye kusaka ushindi ndani ya dakika 90.
“Tunawaheshimu Mbeya City ni timu nzuri ipo wazi ila haitatufanya tuingie uwanjani kwa kujiamini, kila kitu kitakuwa sawa ndani ya uwanja mashabiki watupe sapoti,” amesema.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imecheza jumla ya michezo 18 bila kupoteza, wameshinda michezo 13 na sare tano, huku ikijikusanyia alama 44.