Kocha Mkuu wa Young Africans, Cedric Kaze, anajipanga kuingia sokoni wakati wa dirisha dogo ili kuborsha safu yake ya ushambuliaji, ili kukamilisha azma ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.
Kaze ambaye juzi Jumapili Novemba 15 alikishuhudia kikosi chake kikicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Africans Lyon na kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri, amesema kwa kipindi kifupi alichokaa na timu hiyo amebaini mapungufu hasa kwenye safu ya ushambuliaji kushindwa kuwa na makali.
Amesema kikosi chake kipo vizuri katika idara zote, lakini kinampa changamoto katika safu ya ushambuliaji ambayo inakosa watu wakuweza kuwasumbua mabeki wa timu pinzani.
“Tumekuwa tunashinda mechi zetu, lakini bado hatua watu ambao wanaweza kutia presha kwa wapinzani, tunahitaji kupata watu mbele watakaoweza kupambana kutafuta matokeo,” amesema.
“Katika michezo mingi ukiwamo huu wa kirafiki dhidi ya African Lyon, nimeona jinsi gani washambuliaji wangu wanavyopokonywa mipira na mabeki, hili nalifanyia kazi kwa kipindi hichi, lakini bado nahitaji wachezaji wapambanaji watakaowasumbua mabeki wa timu wapinzani,” alisema kocha huyo.
Hadi sasa safu ya ushambuliaji ya Young Africans imefunga mabao 12 baada ya michezo kumi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku mabeki wakiruhusu mabao matatu pekee.
Dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa Desemba 15, na klabu zote za Ligi Kuu zitautumia muda huo kufanya usajili ili kuboresha vikosi vyao kwa ajili ya kupambana na kutimiza malengo waliojiwekea.