Kocha mkuu wa Young Africans Cedric Kaze amesema anatamani kuanza mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ushindi dhidi ya Tanzania Prisons, baada ya kumaliza mzunguuko wa kwanza pasina kupoteza mchezo wowote.
Kaze ambaye leo anatarajiwa kukamilisha maandalizi ya kikosi chake kabla ya kuwakabili maafande hao wa Jeshi la Magereza kesho Alhamis (Desemba 31), amesema matamanio yake ya kuanza mzunguuko wa pili kwa ushindi, yanatokana na hitaji la kutaka kuweka rekodi ya kipekee tangu alipotua kwenye klabu hiyo, akichukua nafasi ya kocha Zlatko Krmpotic.
Amesema matokeo ya kumaliza mzunguko wa kwanza, huku wakiongoza msimamo wa Ligi Kuu, yanawapa ari ya kuendeleza ushindi mzunguko wa pili, na anaamini mpango huo utakamilika kufuatia wachezaji wake kuwa na hamu ya kupambana kila kukicha.
“Tuna kila sababu ya kushukuru kumaliza mzunguko wa kwanza tukiwa tunaongoza msimamo wa ligi, hii ni kutokana na wachezaji kujitoa na kujitambua kuhakikisha tunapata pointi tatu katika kila mchezo ambazo zimetufikisha hapa.
“Natumaini tutaanza tena vizuri mzunguko wa pili ili tuweze kufanikiwa kufanya vizuri na mwisho wa siku tutwae ubingwa wa ligi,” amesema Kaze.
Hata hivyo, tayari Katibu Mkuu wa Prisons, Ajibu Kifukwe, amesema anakumbuka msimu uliopita Prisons ilikuwa ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hata moja kwenye Ligi Kuu, lakini Young Africans ndiyo ilitibua rekodi hiyo, kwa hiyo na wao wamejipanga kulipiza kisasi kwa kuwaharibia rekodi yao ya kutopoteza pia.
Timu hizo zitashuka Dimba la Nelson Mandela mjini Sumbawanga kesho Alhamis (Desemba 31), zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao moja kwa moja katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.