Vinara wa Ligi Kuu ya England Arsenal Jumapili (April 09) watakabiliana na Liverpool itakayopkuwa nyumbani Anfield, huku The Reds ikisaka nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.
Katika msimamo, Arsenal wanashikilia usukani wakiwa na alama zao 72 baada ya kushuka dimbani mara 29 huku Liverpool wana alama 43 baada ya kucheza mechi 28 na kushika nafasi ya nane.
Manchester United na Newcastle wenyewe watashuka katika viwanja tofauti leo kusaka alama tatu muhimu ili kujiweka katika nafasi nzuri katika ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 20.
Man United inayofundishwa na Meneja Mholanzi, Erik ten Hag wenyewe wako katika nafasi ya nne wakiwa na alama 53 baada ya kushuka dimbani mara 28 sawa na Newcastle ambao pia wana alama kama hizo wakiwa katika nafasi ya tatu.
Frank Lampard ambaye juzi aliteuliwa kuifundisha Chelsea, yeye atakuwa katika benchi la ufundi wakati Chelsea ikiwa mgeni wa Wolves baada ya kocha huyo kurejea Stamford Bridge kama Meneja wa muda katika timu hiyo aliyopata nayo mafanikio makubwa akiwa mchezaji.
Arsenal itasafiri kwenda hadi Anfield ikisaka ushindi wa nane mfululizo katika Ligi Kuu wakikaribia kwa mara ya kwanza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu katika kipindi cha takribani miaka 19.
Klopp hivi karibuni alishuhudia timu yake ikitoka sare ya bila kufungana na Chelsea katikati ya wiki baada ya vipigo vitatu mfululizo katika mashindano yote, akiwapongeza wachezaji wake kwa sare hiyo.
The Gunners, ambao hawajashinda Anfield katika ligi tangu mwaka 2012, inakabiliana na ratiba ngumu mwezi Aprili, huku ikiwa na mchezo dhidi ya Manchester City na Chelsea baadaye mwezi huu. Lakini endapo wataifunga Liverpool na mabingwa watetezi City, iliyo nyuma kwa alama nane nyuma dhidi ya Arsenal huku ikiwa na mchezo mkononi, inaweza kuanza kupoteza matumaini kama inaweza kuwapata wapinzani wao.