Waandishi wa habari kwa makumi wamefukuzwa kazi baada ya kampuni ya Microsoft kuamua kutumia ‘roboti’ (robot) na programu maalum za kompyuta kufanya kazi zao.
Microsoft walikuwa wanatumia waandishi wa habari kutoka wakala wa habari wa Uingereza, Associated Press (AP) kwa makubaliano maalum. Waandishi hao walikuwa wanafanya kazi katika tovuti ya MSN na tovuti nyingine shiriki zinazotumiwa na mamilioni ya raia wa Uingereza kila siku.
Takribani waandishi wa habari 37 waliokuwa wameajiriwa na AP Media, wameelezwa kuwa watapoteza kazi zao ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, kwakuwa hawahitajiki kufanya kazi hizo tena kwani zinaweza kufanywa na roboti. Kazi hizo ni pamoja na kuchagua habari, kuhariri na kuweka kwenye kurasa za mbele za tovuti mbalimbali za MSN.
AP iliwaambia wafanyakai hao kuwa uamuzi wa Microsoft kuhitimisha mikataba yao na kampuni hiyo ulifanywa na kutolewa taarifa ya muda mfupi, kama sehemu hatua ya dunia kuhama kutoka kwenye matumizi ya binadamu na kutumia mifumo ya kompyuta kuhuisha habari ‘automatically’.
Mmoja kati ya waandishi ambao ajira zao zimesitishwa, amekaririwa na The Guardian ya Uingereza akisema, “nimetumia muda mwingi kusoma kuhusu jinsi ambavyo roboti na programu zitakavyochukua kazi zetu, na sasa niko hapa naona uhalisia, kazi yangu imechukuliwa.”
Hata hivyo, alisema kuwa uamuzi huo wa Microsoft una hatari kwakuwa wakati watu wanafanya kazi walikuwa wanachukua tahadhari kubwa na kuzingatia kwa umakini ‘miongozo ya uhariri’, ambayo ilikuwa inahakikisha mtumiaji hakutani na taarifa zisizo sahihi au zenye maudhui yasiyofaa, hususan watoto au vijana wadogo.
Timu ya wafanyakazi kwenye tovuti ya Microsoft hawakuwa wanaandika taarifa kutoka kwenye chanzo asili, bali walikuwa wanachagua habari na kuzihariri kutoka kwenye mashirika mengine ya habari yenye makubaliano maalum na Microsoft.
Kisha, waandishi hao walikuwa wanaweka vichwa vya habari vinavyoendana na tovuti yao. Baada ya habari hiyo kuwekwa kwenye tovuti, Microsoft iligawana mapato ya matangazo na tovuti zilizoandika habari kutoka kwenye chanzo asili (original source).
Polisi wanasa pikipiki 825 zilizoibiwa, waanika mbinu zilizotumiwa na wezi