Hewa ya naitrojeni yenye uwezo wa kuhifadhi mbegu za uzazi za kiume na kike imeanza kutangenezwa katika hospitali ya rufaa ya kanda ya kaskazini (KCMC).
Mwishoni mwa mwaka jana hospitali hiyo ilianzisha huduma ya uzazi kwa watu wenyeshida ya kupata ujauzito ambapo kliniki hufanyika mara moja kwa wiki.
Pamoja na hewa ya naitrojeni, hospitali hiyo pia imeanza kutangeneza hewa safi ya oksijeni ambayo huhitajika kusaidia wagonjwa wenye matatizo ya kupumumua na wale wanaohitaji upasuaji kwa kutumia dawa za usingizi.
Hayo yamewezekana baada ya hospitali hiyo kujenga na kufungua kinu cha kufulia hewa safi ya oksijeni pamoja na ya naitrojeni, kinu hicho kinauwezo wa kuzalisha zaidi ya mitungi 400 kwa siku.
Kaimu Mkurugenzi mtendaji ambaye pia ni mkurugenzi wa huduma za hospitali ya KCMC, Dkt. Sara Urasa amebainisha hayo jana katika ziara ya kampeni ”Tumeboresha sekta ya afya” ambayo imelenga kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano.
” Gesi ya naitrojeni hutumika katika kuhifadhi mbegu za uzazi kwa wale watu ambao wanakabiliwa na matatizo ya uzazi, si tu inasaidia katika huduma za afya ya binadamu, hewa hii hutumika pia na wataalamu wanaoshughulika na afya ya wanyama” amefafanua Dkt. Urasa.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake KCMC, Benjamin Shayo amesema hivi sasa matibabu wanayoweza kutoa kwa wale walioshindwa kupata ujauzito ni kuwapatia dawa za kupevusha mayai.
Amebainisha kuwa wanapokea wanawake wengi walio na umri wa kati ya miaka 30 hadi 42 ambao wanashindwa kupata mimba.