Mshambuliaji wa Sierra Leone Kei Kamara, ametangaza kustaafu soka la kimataifa, licha ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, ambacho jana kilianza kampeni ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika (AFCON 2021) kwa kulazimishwa matokeo ya sare dhidi ya Lesotho.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 35, alitangza maamuzi ya kustaafu soka la kimataifa kabla ya mchezo dhidi ya Lesotho, uliochezwa mjini Free Town.
Kamara anaeitumikia klabu ya Colorado Rapids inayoshiriki ligi kuu ya Marekani MLS, alisema maamuzi yake ya kustaafu soka la kimataifa yamekuja, kufuatia kuchoshwa na mwenendo mbovu wa uendeshaji wa timu ya taifa ya Siera Leone, ambayo inanolewa na kocha kutoka Ghana Sellas Tetteh.
“Ninathibitisha kustaafu soka la kimataifa, nimechoshwa na mwenendo wa uendeshaji wa timu ya taifa,” Kamara aliiambia BBC Sport.
“Nimeitumikia timu yangu ya taifa tangu mwaka 2008, kumekua hakuna maendeleo yoyote, hakuna mipango ya kuiongoza timu ili ifanikishe malengo ya kushiriki fainali kubwa barani Afrika na duniani.”
“Sehemu yoyote duniani soka la vijana limekua likitumika kama mpango wa kufanikisha malengo ya timu ya taifa ya wakubwa, lakini nchini kwangu hakuna jambo kama hilo, na ndio maana kila siku tumekua tunaendelea kufanya vibaya na hatufiki mbali.”
Tayari kocha mkuu wa Siera Leone Sellas Tetteh ameshajaza nafasi ya mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu za Norwich na Middlesbrough zote za England, kwa kumuitwa kikosini Sallieu Tarawallie.
Tetteh amesema anaheshimu maamuzi ya kamara, na daima ataendelea kukumbukwa kwa mchango wake alioutoa kwa muda mrefu, huku akisisitiza hana budi kuendelea na harakati zake za kuifikisha mbali Siera Leone kupitia mchakato wa kusaka nafasi ya kushiriki fainali zijazo za Afrika (AFCON 2021)
“Ninaheshimu maamuzi ya Kamara, niliamini angekua nasi katika kipindi hiki cha harakati za kufuzu fainali za 2021, lakini kujiondoa kwake kikosini na kutangaza kustaafu, ni hatua nzuri kwake, ninamtakia kila la kheri katika shughuli zake za soka upande wa klabu.” Alisema Tetteh
Kikosi cha Siera Leone kitaendelea na mchakato wa kusaka nafasi ya kushiriki fainali za mataifa ya Afrika juma lijalo kwa kucheza mchezo wa pili wa kundi L dhidi ya Benin mjini Porto-Novo.