Jeshi la Mali limetangaza kumuachia huru aliyekuwa Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita ambaye alikamatwa Agosti 18, na kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini humo.
Pamoja na kuachiwa kwa Rais huyo, taarifa zinaeleza kwamba, mwanae Karim Keita ameondoka nchini humo na kwa sasa yuko nje ya nchi.
Viongozi wa mataifa ya Afrika magharibi kutoka kundi la mataifa 15 linalofahamika kama ECOWAS wameshutumu mapinduzi hayo dhidi ya rais aliyechaguliwa na kuweka vikwazo dhidi ya mali, wakifunga mipaka, kuzuia uingiaji wa fedha na kutishia vikwazo zaidi.
Wakati huohuo, mkutano wa pili wa ECOWAS, uliofanyika leo umekubali wazo la Serikali ya Mpito kwa kipindi cha miezi 6, 9 au 12 itakayoongozwa na raia au mwanajeshi mstaafu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi.
Keita aliwekwa kizuizini Agosti 18 wakati kundi la maafisa wa jeshi lilipomkamata na kumpeleka katika kituo cha jeshi cha Kati, kilometa 15 kutoka mji mkuu Bamako ambapo baadaye usiku huo alitangaza kujiuzulu urais wa taifa hilo.