Baada ya kuwa na uhakika wa kumkosa Henock Inonga ‘Varane’, katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, Kocha Mkuu wa Simba SC Robertinho Oliveira, ameanza kumpa madini Beki mzawa Kennedy Juma.
Inonga, amekuwa akiongoza safu ya ulinzi ya Simba SC kwa kushirikiana vema na Mcameroon Fondon Che Malone, ambaye amerithi viatu vya Joash Onyango aliyetimkia Singida Fountain Gate FC.
Lakini Juma lililopita katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union, Inonga alipata majeraha ya mguu wa kulia baada ya kuchezewa rafu mbaya na Haji Ugando, hivyo hatokuwa sehemu ya kikosi kitakachoivaa Power Daynamos Jumapili (Oktoba Mosi) kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Kwa kulitambua hilo, Kocha Robertinho, ambaye ana kazi kubwa ya kuhakikisha Simba SC inapata matokeo ya jumla ili kutinga hatua ya makundi baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo wa kwanza nchini Zambia, ameanza kumpika vilivyo Kennedy ili kupata muunganiko mzuri na Malone.
Akizungumza jijini Dar es salaam Robertinho amesema kwa sasa ameanza mchakato wa kumjenga Kennedy kuelekea mchezo huo kutokana na kumkosa Inonga.
“Tunaendelea kuweka mikakati na mipango yetu sawa katika uwanja wa mazoezi kuelekea katika mchezo wetu muhimu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kutokana na matokeo ya mchezo wetu wa Mkondo wa kwanza tuliocheza Zambia.
“Nimeanza kumtengeneza Juma Kennedy ili aweze kucheza kati na Che Malone, naamini atafanva vizuri kwa sababu si mara ya kwanza, amefanya hivyo katika mechi za Ngao ya Jamii mpaka tukaibeba.
“Nimeamza kumuweka sawa kulingana na presha ya mchezo wenyewe pamoja na kuongea naye kila mara ili kuwa kwenye kiwango bora cha kuweza kupata matokeo,” alisema Robertinho.
Amesema anaimani kikosi chake kitafanya vizuri kwa sababu wameanza mazoezi kuelekea mchezo wao wa marudiano dhidi ya Power Dynamos lengo likiwa ni kupata ushindi na kufuzu hatua ya makundi.
Inonga ambaye aliumia katika Uwanja wa Uhuru, Dar es salaam na kushonwa nyuzi 13 katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara, ambao Simba SC iliondoka na ushindi wa mabao 3-0, imeelezwa pia ataukosa mchezo ujao wa ligi hiyo ugenini dhidi ya Tanzania Prisons.
Simba SC inahitaji kupata ushindi wowote, suluhu ama sare ya bao 1-1, ili kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, matokeo ambayo wakiyapata watakuwa katika mwendo mzuri wa kuelekea kutimiza malengo yao kucheza nusu fainali ya mi- chuano hiyo msimu huu.
Hata hivyo, katika kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa imara na safu yake hiyo ya ulinzi inapata muunganiko mzuri, mapema leo Jumanne (Septemba 26) Simba SC imecheza mchezo wa Kirafiki dhidi ya Pan Africans katika Uwanja wa Mo Simba Arena jijini Dar es salaam.
Matokeo ya mchezo huo Simba SC imechomoza na ushindi wa mabao 4-0, yakifungwa na Saido Ntibazonkiza, Kibu Dennis, Esomba Onana na Moses Phiri.