Wakati baadhi ya Wanasiasa wa Upinzani na Wanaharakati wakipinga mpango wa kampuni ya DP World ya Dubai kuwekeza kwenye Bandari ya Dar es Salaam, Kenya imetangaza maamuzi ya kusaini mikataba ya uwekezaji na Umoja wa Falme za Kiarabu – UAE.
Rais William Ruto ametangaza kupitia akaunti yake ya Twitter leo kuwa amefanya mazungumzo kwenye Ikulu ya Nairobi, Kenya, na Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE, Sheikh Shakhboot bin Nahyan Al Nahyan, kujadili fursa za uwekezaji.
“Kenya na Umoja wa Falme za Kiarabu watasaini makubaliano ya uwekezaji ambayo yataimarisha uhusiano kati ya nchi zetu na kutengeneza fursa kwa wananchi wetu,” Rais Ruto alisema.
Alisema kuwa makubaliano hayo ya uwekezaji kati ya Kenya na UAE yatajikita kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo miundombinu ya usafirishaji huku Waziri Shakhboot wa UAE pia amefanya ziara kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kukutana na Rais Felix Tshisekedi kujadiliana kuhusu fursa za uwekezaji.
Zambia pia nayo imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuvutia uwekezaji kutoka UAE na Serikali ya Ruto imeanza jitihada kubwa ya kutafuta wawekezaji binafsi kama DP World kwenye bandari zake na miundombinu mingine ya usafirishaji.
Kampuni ya DP World ya Dubai, ambayo ndiyo kitovu cha uchumi cha UAE, mwaka jana ilifanya mazungumzo na Serikali iliyopita ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusu uendeshaji wa bandari za Kenya, ikiwemo Mombasa.
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Kenya mwaka jana, umoja wa upinzani wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Ruto ulipinga mpango wa Rais Kenyatta wa kujadiliana na DP World na kumshutumu kuwa anapanga kuuza bandari.
Baada ya kuingia madarakani, serikali ya Rais Ruto imegeuka na kufufua mpango wa kutaka kukodisha bandari za nchi hiyo kwa wawekezaji binafsi kama DP World ili kuongeza ufanisi wakati Kenya wanachukua hatua za haraka kuvutia uwekezaji kutoka Dubai, nchini Tanzania kumekuwa na mjadala mrefu kuhusu mpango wa kampuni ya DP World kufanya uwekezaji kwenye bandari ya Dar es Salaam.
Licha ya kelele nyingi zinayopigwa na viongozi wa upinzani na wanaharakati, uwekezaji binafsi kwenye bandari siyo jambo geni nchini Tanzania na Kampuni ya TICTS yenye makao makuu Hong Kong, ilipewa mkataba kuendesha eneo la makontena la bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 22 chini ya uongozi wa marais Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli.
Mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Marekani, Uingereza, China, Canada, Uholanzi, Korea Kusini, Afrika Kusini, Brazil, Norway, Uswisi, Ujerumani, Ufaransa, India, Uturuki, Australia, Msumbiji, Senegal, Misri na Rwanda yameingia mkataba na DP World kuendesha bandari zao.
Rais Samia Suluhu Hassan ameonya hivi karibuni kuwa iwapo Tanzania haitachukua fursa ya uwekezaji binafsi kwenye bandari ya Dar es Salaam kwa haraka, inaweza kupoteza fursa hiyo na ikachukuliwa na nchi jirani.
Kumekuwa na upotoshaji mkubwa kwenye mjadala wa uwekezaji binafsi katika bandari ya Dar es Salaam, huku baadhi ya wanasiasa wakisambaza uongo kuwa bandari imeuzwa ili kuibua taharuki kwa wananchi.