Wakili wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), George Murugu amesema tume hiyo iliharakisha tangazo la matokeo ya urais kutokana na wasiwasi wa usalama wa makamsihna wake na wafanyakazi kiujumla.
Wakili Murugu, ameyasema hayo wakati alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa majaji wa mahakama, kuhusu swali lililohoji uharakishaji wa kutangaza matokeo bila kujumlisha matokeo mengine ambayo tayari yalikuwa yamethibitishwa.
Amesema, tume hiyo pia ilifanya uamuzi wa kutotangaza majimbo 27 yaliyosalia licha ya kujumlishwa na kuthibitishwa na kwamba matokeo yalikuwa tayari kwa kutangazwa na Profesa Abdi Guliye, lakini kutokana na tishio, waliamua kutangaza matokeo ya urais pekee.
“Unyanyasaji wa mara kwa mara ambao wafanyakazi wa tume hiyo walikuwa wakikabiliana nao, ambao ni pamoja na kukamatwa na vitisho ndio ulisababisha uamuzi huo kufanyika ili kuondoa kadhia zilizokuwepo,” amebainisha Murugu.
Hata hivyo, Murugu ameongeza kuwa, ” Mkuu wa IEBC, Chebukati alizingatia kuhusu usalama wa wafanyAkazi wake ambao wakati huo walikuwa wakikabiliwa na tishio la kukamatwa, kutekwa nyara na kujeruhiwa wakiwemo makamishna.”