Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati ameripotiwa kufanya mkutano usiku kwa saa tatu Agosti 14 na makamishna wote, wakala wa vyama, manaibu wao na makatibu wao katika ukumbi wa Bomas of Kenya.
Taarifa za ndani zinazofikia vyombo vya habari zinasema sababu za mkutano huo wa Jumapili, Agosti 14 usiku, zilikuwa kupunguza vurugu zilizoshuhudiwa katika ukumbi huo ambao ndiyo Kituo cha Kitaifa cha Kujumlisha Kura.
Mawakala hao wakuu walielekezwa na IEBC kuwafahamisha wanachama wa vyama vyao kukaa kimya kwa muda uliobaki kabla ya kutangazwa kwa Mgombea alieshinda kiti cha Urais.
Chebukati amesema wale ambao hawatatii amri hiyo watafukuzwa ukumbini humo.
Siku ya Ijumaa na Jumapili zilishuhudiwa vurugu huku wakala wa pande zote kati ya Azimio na Kenya Kwanza wakidai kuna wizi wa kura wakati wa zoezi la ujumuishaji na utathmini ukiendelea katika ukumbi wa Bomas.