Jaji Mkuu wa Kenya David Maraga, amemshauri rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta, kulivunja bunge la kitaifa na lile la Senate, baada ya wabunge kushindwa kupitisha sheria ya jinsia kuhusu theluthi mbili.
Katiba ya Kenya inataka sheria hiyo kuwepo ili kudhibiti jinsia bungeni kutotawala katika nyadhifa za uteuzi, na kwa miaka 10 sasa wabunge ambao wengi ni wakiume, wameshindwa kupitisha sheria hiyo.
Hatua hiyo ya Jaji Mkuu inaungwa mkono na chama cha Mawakili nchini humo na idadi kubwa ya wabunge wanawake ambao ni asilimia 22 katika baraza la bunge la kitaifa na asilimia 22 katika Bunge la Senate.
Jaji Maraga amesema wabunge na maseneta wamekwenda kinyume na Katiba ya mwaka 2010 iliyowataka kutunga sheria hiyo.
Spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi ameiambia Televisheni ya nchi hiyo ya Citizen kuwa, hatima ya Bunge hilo sasa ipo mikononi mwa rais Kenyatta.