Baadhi ya vituo vya Luninga vimeacha kutangaza makadirio ya matokeo ya uchaguzi uliofanyika siku ya Jumanne Agosti 9, 2022 licha la zoezi hilo kuendelea kutolewa na mawakala wa wa tume ya IEBC nchini Kenya.
Siku moja baada ya uchaguzi, vituo vya runinga vya Kenya vilianza kutangaza matokeo yasiyopungua, yanayobadilikabadilika na wakati mwingine yakipingana kulingana na hesabu zao.
Makadirio hayo yalikuwa yakitolewa mbashara kuonesha hali ya ushindani mkali wa wagombea wawili kati ya wanne wanaowania urais wa Kenya yaani Raila Odinga, ambaye anaungwa mkono na Rais Kenyatta katika uchaguzi huo, na William Ruto, Makamu wa Rais anayemaliza muda wake.
Tume Huru ya Uchaguzi na mipaka nchini Kenya (IEBC), inatarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais Agosti 16, 2022, ambayo yataamua ni nani atamrithi Uhuru Kenyatta, ambaye amekuwa madarakani tangu 2013.
Taairfa ya IEBC, imesema waliojitokeza kupiga kura siku ya Jumanne Agosti 9, walikuwa ni zaidi ya asilimia 65, idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na ile ya asilimia 78 ya uchaguzi uliopita wa Agosti mwaka 2017.
Kwa mwaka huu, IEBC iko chini ya shinikizo maalum la utendaji kazi baada ya Mahakama ya Juu nchini humo kubatilisha uchaguzi wa urais wa mwaka wa 2017 kwa makosa.